Real Madrid yamchukua kocha Álvaro Arbeloa kuchukua nafasi ya Xabi Alonso

Madrid (AP) —
Real Madrid imemwondoa kocha Xabi Alonso na kumchukua kocha wa timu B, Álvaro Arbeloa, kuiongoza timu ya kwanza kuanzia Jumatatu.

Katika taarifa yake, Real Madrid ilisema kuwa Alonso ameondoka kwa makubaliano ya pande zote mbili.

Tangazo hilo lilitolewa siku moja baada ya Real Madrid kupoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Barcelona katika fainali ya Kombe la Super la Hispania lililofanyika Saudi Arabia. Hatua hiyo imehitimisha kipindi chenye misukosuko kilichodumu kwa chini ya miezi minane kwa kiungo huyo wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Hispania.

“Real Madrid inapenda kutangaza kuwa, kwa makubaliano ya pamoja kati ya klabu na Xabi Alonso, imeamuliwa kumaliza kipindi chake kama kocha wa timu ya kwanza,” ilisema taarifa ya klabu.
“Xabi Alonso ataendelea kuwa na upendo na heshima ya Madridistas wote kwa sababu yeye ni gwiji wa Real Madrid na amekuwa akiuwakilisha daima misingi na maadili ya klabu yetu. Real Madrid itabaki kuwa nyumbani kwake siku zote.”